IFLA

As of 22 April 2009 this website is 'frozen' in time — see the current IFLA websites

This old website and all of its content will stay on as archive – http://archive.ifla.org

IFLANET home - International Federation of Library Associations and InstitutionsActivities and ServicesSearchContacts

School Libraries and Resource Centers Section

ILANI YA MAKTABA ZA SHULE YA IFLA/UNESCO

(Kiswahili translation of IFLA/UNESCO School Library Manifesto)

MAKTABA YA SHULE KATIKA KUFUNDISHIA NA KUJIFUNZA

Maktaba ya shule hutoa habari na dhana ambazo ni za msingi kwa mafanikio ya jamii ya kisasa ambayo kimsingi inategemea zaidi habari na maarifa. Maktaba ya shule huwapa wanafunzi mbinu za kujifunza katika maisha na kukuza ubunifu wao ili kuwawezesha kuishi kama raia wanaowajibika.

MAELEKEZO YA MAKTABA YA SHULE:

Maktaba ya shule hutoa huduma za kujifunzia, vitabu na zana zinazowawezesha wanachama wote wa jumuiya ya shule kuwa na umakinifu na watumiaji hodari wa habari zinazotokana na miundo mbalimbali na njia za mawasiliano zenye viungo muhimu katika maktaba na mtandao wa habari kufuatana na kanuni za Ilani ya Maktaba ya Umma ya UNESCO.

Watumishi wa maktaba wanasaidia katika matumizi ya vitabu na vyanzo vingine vya habari kuanzia vitabu vya hadithi za kubuni, maandiko ya hati, habari za machapisho na elektroni zilizopo katika maktaba ya shule na nje. Ni muhimu mahitaji haya yajazie na kurutubisha vitabu vya kiada, nyenzo za kufudishia na mbinu zake.

Imedhihirika kwamba walimu na wakutubi wanapofanya kazi kwa kushirikiana, wanafunzi hupata mafanikio zaidi katika kusoma na kuandika, uwezo wa kujifunza, uwezo wa kutatua matatizo pamoja na kuwasiliana na mbinu za upashanaji habari kwa njia za teknolojia.

Ni lazima huduma za maktaba ya shule zitolewe kwa usawa bila kuangalia umri, rangi, mume au mke, dini, taifa, lugha, taaluma au cheo katika jamii. Vile vile ni lazima huduma maalum na vifaa zitolewe kwa wote ambao hawapati fursa ya kutumia huduma za kawaida za maktaba.

Fursa ya kupata huduma za maktaba ni lazima zikuabaliane na tamko la haki na uhuru wa binandamu la Umoja wa Mataifa na sio kufuatana na itikadi za kisiasa, dini au misukumo ya kibiashara.

SHERIA YA UTOAJI FEDHA NA MITANDAO YAKE:

Maktaba ya shule ni muhimu kwa mikakati ya muda mrefu kwa ajili ya mafunzo, elimu, na mendeleo ya tamaduni za kijamii yanayotokana na upashanaji wa habari na maendeleo ya kiuchumi. Ni lazima mamlaka za serikali za mitaa, mikoa na taifa ziwe na sheria na sera maalumu zitakazotetea mipango ya huduma za maktaba. Vile vile yawepo mafungu ya fedha ya kutosha na ya kudumu kwa ajili ya maendeleo ya watumishi, teknolojia na vifaa, na utipatikanaji wake uwe wa rahisi na bure.

Maktaba ya shule inatakiwa ishiriki katika shughuli za maktaba za mitaa, mikoa, taifa na mitandao yake ya utoaji wa habari.

Makusudio ya maktaba ya shule ni lazima yakubalike na kudumishwa mahala popote ambapo maktaba ya shule ina ubia wa vifaa na rasilimali za maktaba nyingine mathalani maktaba za umma.

MALENGO YA MAKTABA YA SHULE:

Maktaba ya shule ni sehemu muhimu kwa maendeleo ya elimu.

Pamoja na kuwa ni kiini cha huduma za maktaba ya shule, dondoo zifuatazo ni muhimu katika maendeleo ya elimu, upashanaji wa habari, kufundisha, kujifunza na utamaduni.
  • Kusaidia na kuboresha malengo ya elimu kama yalivyoorodheshwa katika misheni ya shule na mitalaa.
  • Tabia za watoto za kupenda kusoma na kujifunza pamoja na kutumia maktaba ziendelezwe na kudumishwa maishani yao.
  • Kutoa fursa ya kupata ozoefu wa kuvumbua na kutumia habari kwa ajili ya elimu, uelewaji, ubunifu na ridhaa.
  • Wanafunzi wasaidiwe katika shughuli zao za kujifunza na kupata umahiri katika kutathimini na kutumia habari, bila kujali taratibu/fani, muundo au njia ya upatikanaji wa habari pamoja na kiwango cha hisi katiaka njia za mawasiliano za jumuiya.
  • Kutoa fursa kwa upatikanaji wa rasilimali za mitaa, mikoa, kitaifa na kimataifa na nafasi ambazo zinawawezesha wanafunzi kupata mawazo mbalimbali, uzoefu na maoni.
  • Kuandaa shughuli zinazohamasisha hisia ya utamaduni na elimu ya jamii.
  • Kushirikiana kikazi na wanafunzi, walimu, watawala na wazazi ili kufikia misheni ya shule.
  • Kuweka wazi dhana ya kuwa uhuru wa fikra na upatikanaji wa habari ni vitu muhimu kwa uraia wa kuwajibika na utekelezaji wa demokrasia.
  • Kukuza usomaji, rasilimali na huduma za maktaba ya shule kwa jumuiya ya shule na nje.

Maktaba ya shule itatekeleza shughuli hizi kwa kuanzisha sera na huduma nzuri, kuchagua na kununua rasilimali husika, kuandaa mahali pa kusomea ili kutoa fursa ya kifikra itakayowawezesha watumiaji kupata vyanzo vya habari, pamoja na nyenzo za kufundishia, na vile vile kuajiri watumishi wenye taaluma.

WATUMISHI:

Mkutubi wa shule ni mtaalam mweza atakayewajibika katika kupanga na kuendesha shughuli za maktaba ya shule, akisaidiwa na watumishi wengine wa kutosha iwezekanavyo, akifanyakazi pamoja na wanajumuiya ya shule nzima na atakuwa kiungo muhimu kwa maktaba za umma na nyinginezo.

Wajibu wa wakutubi wa shule utabadilika kutegemea na malengo ya fedha, mitalaa na mbinu za ufundishaji katika mashule, kufuatana na hali ya fedha na mfumo wa sheria. Katika taratibu maalum, kuna maeneo ya kawaida ya elimu ambayo ni muhimu kwa wakutubi wa shule kuweza kuanzisha na kuendesha vizuri huduma za maktaba za shule,

Ili kuwa sambamba na mabadiliko ya maendeleo ya mitandao, wakutubi wa shule lazima wawe wastadi katika kupanga na kufundisha mbinu mbalimbali za utumiaji wa habari kwa wnafunzi pamoja na walimu. Kwa hiyo ni lazima wajiendeleze katika taaluma yao.

UTENDAJI NA UENDESHAJI:

Ili kuleta matokeo yanayotakiwa na uendeshaji wa kuwajibikaji inabidi:
  • Iundwe sera ya huduma ya maktaba za shule amabayo itafafanua malengo, kipaumbele na huduma zake kufuatana na mitalaa ya shule.
  • Maktaba ya shule lazima ipangwe na kudumishwa kwa mujibu wa viwango vya kitaalamu.
  • Huduma za maktaba lazima zipatikane kwa jumuia nzima ya shule na ziendeshwe katika mazingira ya jumuiya ya mahali.
  • Ushirikiano baina ya walimu na wakutubi wa shule, uongozi wa ngazi za juu wa shule, watawala, wazazi pamoja na wakutubi wengine na wataalam wa habari, na vikundi vya jumuiya lazima utiwe moyo.

UTEKELEZAJI WA ILANI:

Serikali, kupitia wizara zake za elimu, zinaombwa kutengeneza mikakati, sera na mipango ambayo itatekeleza maadili ya ilani hii.

Mipango itapaswa ijumuishe usambazaji wa ilani yenyewe kwa mafunzo ya awali na ya kuendelea kwa wakutubi na walimu.

Wenye mamlaka ya kuota maamuzi katika ngazi za taifa na mitaa na jumuiya za maktaba ulimwenguni, wanahimizwa kutekeleza maadili yaliyoelezwa katika ilani hii.

Ilani hii ilitayarishwa na Mwungano wa kimataifa wa vyama vya Maktaba na Taasisi (International Federation of Library Associations and Institutions) na kuthibitishwa na Umoja wa Mataifa wa Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) katika mkutano wake mkuu uliofanyika mwezi Novemba 1999.

Kimechapishwa na Maktaba ya Taifa ya Kanada

Imetafsiriwa kwa Kiswahili na Felix K. Tawete na Dr. P.A. Lyoka wa Chuo Kikuu cha Botswana, Gaborone January 2005. Haki za kutafsiri chapisho hili zimehifadhiwa.